Bingwa wa Jumuia ya Madola katika mita 100 Ferdinand Omanyala, atawaongoza wa Wakenya kesho katika mkondo wa pili wa mashindano ya Diamond League mjini Shanghai, China.
Omanyala anayejivunia muda wa sekunde 10.0, msimu huu atamenyana na mshindi wa nishani ya fedha ya Olilimpiki katika mita 100 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti Akani Simbine, wa Afrika Kusini, ambaye tayari amemshinda mara mbili msimu huu.
Wengine watakaoshiriki mita 100 ni mshindi wa nishani ya fedha ya Olimpiki katika mita 100, Kishane Thompson wa Jamaica, na bingwa wa Olimpiki wa mita 200, Letsile Tebogo wa Botswana, miongoni mwa washiriki wengine.
Omanyala alifungua msimu kwa kumaliza wa pili katika mashindano ya Botswana Grand Prix, akisajili sekunde 10.0, nyuma ya Simbine mwezi jana, kabla ya kumaliza tena wa pili Jumamosi iliyopita katika mkomdo wa Xiamen, Diamond League kwa sekunde 10.13.
Mshindi wa nishani ya shaba ya Olimpiki katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji Abraham Kibiwot, bingwa wa dunia kwa chipukizi Edmund Serem, mshindi wa nishani ya shaba katika michezo ya Afrika, Simon Koech na Wilberforce Kones watashindana na mshindi wa mkondo wa Xiamen, Samuel Firehu.
Kwenye fainali ya mita 5,000, bingwa wa zamani wa dunia kwa chipukizi Benson Kiplangat, Samuel Chebolei, Nicholas Kimeli Kipkorir na Cornelius Kemboi watashiriki.