Waziri wa elimu Julius Migos Ogamba amepongeza kazi inayotekelezwa na taasisi za mafunzo ya kiufundi nchini almaarufu TVETs.
Waziri Ogamba alikuwa akizungumza katika taasisi kitaifa ya mafunzo ya kiufundi ya Meru katika awamu ya 6 ya mahafali ambapo wahitimu 3,370 walihitimu katika fani mbalimbali.
Ogamba alisema idadi kubwa ya waliohitimu leo ni ushahidi tosha wa uwezo unaokua wa taasisi hiyo ya kitaifa ya Meru katika kuzalisha wahitimu wenye umahiri, walio tayari kuingia katika ulimwengu wa kazi.
Alisema ubunifu unaofanywa na taasisi hiyo kama vile utengenezaji wa unga wa ndizi chini ya nembo iliyosajiliwa, mapipa ya kisasa ya taka na kikaushio cha jua kwa biashara ya kilimo, vinaonyesha wazi nguvu ya ujuzi wa kivitendo katika kukabili changamoto halisi za maisha.
Waziri alisema kwamba ubunifu huu unaendana kikamilifu na dhamira ya wizara ya kuwa na mfumo wa TVET unaotoa suluhisho za vitendo kwa kipaumbele cha maendeleo nchini Kenya.
Ogamba alisema zaidi kuwa ametiwa moyo na utendaji bora wa chuo cha kitaifa cha ufundi cha Meru katika matamasha mbalimbali ya TVET ambapo taasisi hiyo imekuwa ikionyesha ubunifu wa kipekee na kuibuka miongoni mwa wanaofanya vizuri kitaifa.
Alipongeza uongozi wa taasisi hiyo kwa kukumbatia mfumo wa elimu na mafunzo ya msingi wa umahiri almaarufu CBET, akisema kupitia CBET, mkazo umehamishwa kutoka kwa kile wanachojua wanafunzi hadi kile ambacho wanaweza kufanya.
Waziri huyo wa Elimu alisema kama wizara, wanaendelea kubadilisha vituo vya TVET kuwa injini inayoendesha ukuaji wa viwanda na maendeleo endelevu nchini Kenya.
Kulingana naye ajenda ya mageuzi ya wizara inategemea nguzo kadhaa kama vile kuimarisha utekelezaji katika taasisi zote za TVET ili kuhakikisha mafunzo yanakidhi mahitaji ya soko la ajira.
Pili, wizara inapanua mfumo wa mafunzo pacha unaochanganya masomo darasani na uzoefu wa viwandani.
Ogamba aliushukuru uongozi wa taasisi zote za TVET kwa kujitolea kuingiza teknolojia, akiongeza kuwa kama wizara wanakumbatia Akili Bandia na mafunzo ya kidijitali kuboresha mbinu za kujifunza.
Alisema wizara inawekeza katika miundombinu ya kisasa, vifaa vya kidijitali na vitendea kazi katika Vyuo vyote vya Kitaifa vya Ufundi.
CS pia alibainisha kuwa wizara inakagua upya mfumo wake wa ufadhili ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi stahiki anakosa mafunzo kwa sababu ya changamoto za kifedha.