Afisi ya Mkurugenzi wa mashtaka ya umma ametetea uamuzi wake wa kuwafungulia mashtaka chini ya sheria za ugaidi, baadhi ya waliotiwa nguvuni kwa kushiriki kwenye maandamano yalioshuhudiwa hapa nchini, huku kukiwa na malalamishi kutoka kwa upinzani, mashirika ya kijamii na wananchi.
Kulingana na afisi hiyo, mashtaka hayo yanazingatia sheria na usalama wa kitaifa na wala hayana msukumo wowote wa kisiasa.
Taarifa hiyo iliyotolewa Jumatatu jioni, ilisisitiza kuwa ilitumia sheria ya kukabili ugaidi baada ya uchunguzi kudokeza kuwa visa vya kushambuliwa kwa taasisi za serikali wakati wa maandamano Juni 25,2025 na yale ya Julai 7, 2025, vilikuwa vimepangwa.
“Mashtaka hayo chini ya sheria za kuzuia ugaidi, yanapaswa kueleweka kupitia mifumo ya sheria na usalama wa taifa badala ya kutafsiriwa kama njama ya kukandamiza wanaojieleza kisiasa,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha afisi hiyo ilisema ghasia zilizoshuhudiwa zilikusudiwa kuharibu taasisi za serikali na kuzua hofu miongoni mwa wananchi, hatua zinazopaswa kukabiliwa na sheria za ugaidi.