Chama cha ODM kimeazimia kuendelea kufanya kazi na serikali ya Rais William Ruto katika hatua kinachosema inakusudia kuleta uthabiti nchini.
Azimio hilo limeafikiwa baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kukutana leo Jumanne.
“Kwamba chama cha ODM kinaunga mkono msimamo wa kiongozi wa chama Raila Odinga kufanya kazi na utawala wa Kenya Kwanza ili kuleta uthabiti nchini na kubuni mazingira wezeshi ya Wakenya kuangazia malalamishi yao kupitia njia za kidemokrasia na kikatiba,” lilielezea azimio namba moja kati ya maazimio saba yaliyoafikiwa wakati wa mkutano huo.
Kamati hiyo pia imependekeza kubuniwa kwa kamati ya kiufundi itakayosimamia utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano (MoU) wenye hoja 10 uliotiwa saini kati ya ODM na chama cha UDA.
“Kamati ilitambua kutokuwepo kwa kamati kama hiyo ya kiufundi, ambayo ipo kwenye MoU, kama kitu kinachokosekana katika utekelezaji wa makubaliano hayo,” azimio namba mbili lilielezea zaidi.
Na hakikukomea hapo. Chama chama ODM pia kikitoa wito wa kutekelezwa kwa ripoti ya Kamati ya Maridhiano ya Kitaifa (NADCO), ripoti ambayo utekelezaji wake umekuwa mgumu sawia na kutafuta maji jangwani tangu ilipotayarishwa mwaka 2023.
Kumekuwa na hali ya migawanyiko katika chama ODM siku za hivi karibuni huku baadhi ya wanachama wakikosoa vikali ndoa kati ya ODM na UDA.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amekuwa mstari wa mbele kuikosoa ndoa hiyo akitilia shaka ni kwa misingi gani chama hicho ambacho wakati mmoja kilifahamika kwa kupigania maslahi ya Wakenya kimeazimia kufanya kazi na utawala wa Kenya Kwanza anadai unawakandamiza Wakenya.
Kamati Kuu ya ODM ikionkena kufahamu kuwa misimamo ya wanachama wake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 inaonekana kutofautiana.
“Ingawa wanachama waliwasili hapa wakiwa na misimamo tofauti juu ya masuala mengi ndani ya chama na nchi, kamati iliziba tofauti hizo na kuleta umoja chamani na kuelekeza shabaha kwa suala la kuhakikisha ODM inaendelea kuwa mtumishi mwaminifu kwa watu na nchi, ikichukua hatua zinazokidhi maslahi bora ya wafuasi wake na nchi na kujitolea kwa ajenda ya mabadiliko ya kitaifa na uthabiti.”