Shirika la Nihon Hidankyo la Japani limelimbikiziwa rundo la pongezi kwa kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu.
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amelipongeza shirika hilo kwa kutunukiwa tuzo hiyo kupitia ujumbe alioutuma katika mitandao ya kijamii.
Wakati wa utawala wake, Obama alipigania dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia na kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2009.
“Wakati huu ambapo tishio la silaha za nyuklia linaongezeka na miiko dhidi ya kutishia matumizi yake inadhoofika, kazi ya Nihon Hidankyo inatukumbusha kuwa silaha hizi zina madhara makubwa kwa binadamu, na kwamba kuipigania dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia ni sehemu muhimu ya kuhakikisha tunawaacha watoto wetu kwenye dunia ambayo ni salama zaidi,” alisema Obama katika ujumbe wake.
Obama alilisifu shirika la Nihon Hidankyo akisema kuwa “limejenga vuguvugu lenye nguvu kutokana na janga binafsi na kusisitizia ubinadamu wetu sote.”
Shirika hilo linajumuisha manusura wa mashambulizi ya mabomu ya atomiki yaliyotekelezwa katika miji ya Hiroshima na Nagasaki mwaka 1945.