Nyota wa TikTok Cecilia Achieng afariki katika ajali

Marion Bosire
2 Min Read

Cecilia Achieng raia wa Kenya wa umri wa miaka 23 ambaye alikuwa ameanza kuwa na ushawishi mkubwa kwenye mtandao wa TikTok, alifariki katika ajali.

Achieng anaripotiwa kugongwa na gari kando ya barabara ya Thika alipokuwa akijaribu kuvuka barabara akiwa amelewa.

Kulingana na ripoti za polisi, Cecilia ambaye alikuwa amekamilisha masomo yake katika chuo Kikuu cha Mount Kenya, alikuwa ametoka kwa rafiki yake wa kiume huko Ruiru na alitakiwa kufikishwa nyumbani.

Rafiki huyo alikuwa ameagiza teksi ya mtandaoni imchukue, lakini dereva wa teksi hiyo anasema msichana huyo alikosa nidhamu muda mfupi baada yao kuanza safari.

Dereva huyo alielezea kwamba walisonga kama kilomita moja kutoka eneo ambalo alimchukua kisha Cecilia akaanza kupiga kelele ndani ya teksi na hata kujaribu kumshika shati.

Jamaa huyo anasema alilazimika kusimamisha gari na kumpigia simu mwanamume aliyeagiza teksi aje kumchukua. Mwanamume huyo alikataa kufika eneo la tukio, na anadaiwa kumwelekeza dereva huyo amuache Cecilia.

“Aliniambia nimuache kwenye barabara kuu, akisema yeye ni mtu mzima na angeweza kujitunza” dereva alieleza.

Muda mfupi baada ya dereva kuondoka, Cecilia alijaribu kuvuka barabara ambapo aligongwa vibaya na gari lililokuwa likija na kufa papo hapo.

Dereva aliyehusika katika ajali hiyo alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Juja, ambapo uchunguzi wa tukio hilo la kusikitisha unaendelea.

Share This Article