Tume ya kutetea haki za binadamu nchini India, imesema inachunguza ripoti ambapo zaidi ya wanafunzi 100 waliathirika kiafya, walipokula chakula cha mchana kinachodaiwa kuwa na nyoka aliyefariki.
“Imeripotiwa kuwa mpishi aliwapa wanafunzi chakula baada ya kutoa nyoka alitefariki ndani yake,” Ilisema Tume ya Taifa ya Kutetea Haki za Binadamu( NHRC), kupitia kwa taarifa.
Kulingana na tume hiyo, wanafunzi walipewa chakula hicho juma lililopita katika shule moja ya umma katika mji wa Mokama ulio katika eneo la Bihar, ambao ni miongoni mwa miji maskini zaidi nchini humo.
NHRC, ilitaka maafisa wa serikali na polisi kuchunguza swala hilo, lililosababisha zaidi ya wanafunzi 100 kuwa wagonjwa.
Kisa hicho kilisababisha maandamano kutoka kwa wazazi wa wanafunzi hao waliokuwa na hamaki.
Mamilioni ya wanafunzi katika shule za serikali nchini India hupewa chakula cha mchana bila malipo, kama njia moja ya kuwahimiza wanafunzi kuendelea na masomo.
Aidha tume hiyo ilisema iwapo madai hayo ni ya kweli, basi huo ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wanafunzi hao.
Mnamo mwaka 2013, wanafunzi 23 walifariki baada ya kupewa chakula kilichokuwa na dawa za kuuwa wadudu katika wilaya ya Saran, eneo la Bihar.