Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Joseph Mbugua ametangaza kuwa serikali iko katika hatua za awali za kubuni njia ya watembea kwa miguu katika Daraja la Riverside, linalojulikana kwa hatari yake.
Daraja hilo lipo kwenye mpaka wa kaunti za Nyandarua na Laikipia.
Akizungumza wakati wa ziara katika daraja hilo — linalohudumia maeneo yenye watu wengi kama wadi za Igwamiti na Gatimu katika kaunti ya Laikipia Magharibi, pamoja na Ol Jororok katika kaunti ya Nyandarua, Mbugua alikiri changamoto za muda mrefu ambazo zimekuwa zikiwakumba watembea kwa miguu na madereva.
Alisema watumiaji wa daraja hilo mara nyingi hulazimika kupigania nafasi ndogo, wakijaribu kuepuka kugongana, hali ambayo imekuwa tishio kwa usalama wa wote.

Mhandisi Mbugua aliwahakikishia wakazi kuwa serikali imejitolea kujenga daraja la waenda kwa miguu kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Uamuzi huu umetokana na shinikizo kutoka kwa wananchi pamoja na maombi ya dhati kutoka kwa wazazi na wanafunzi, wakitaka serikali kulijenga upya daraja hilo ili kuwa na sehemu salama ya kutembea.

Wakazi wa maeneo hayo walielezea masaibu yao ya kuvuka daraja hilo huku wakiwa kwenye hatari ya kuangamia.
Baadhi walisimulia hadithi za kupoteza wapendwa wao kwenye ajali za barabarani, huku wengine wakieleza jinsi matukio ya ajali yamekuwa ya mara kwa mara kutokana na ukosefu wa njia ya waenda kwa miguu.
Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa, mara tu mradi huo utakapokamilika, njia hiyo mpya ya waenda kwa miguu itasaidia pakubwa kupunguza ajali na kuokoa maisha kwa kutenganisha watembea kwa miguu na magari.
Mradi huo unatarajiwa kuleta afueni kubwa kwa jamii na kuboresha usalama wa barabarani katika eneo hilo.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara kote nchini.