Niko tayari kuhudumia Bungoma, asema Tim Wanyonyi

Martin Mwanje
1 Min Read
Tim Wanyonyi - Mbunge wa Westlands

Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi anasema yuko tayari kuongoza kaunti ya Bungoma. 

Wanyonyi ametangaza kuwa atagombea wadhifa wa Ugavana wa kaunti hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Juhudi zake za kugombea wadhifa huo katika kaunti ya Nairobi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 ziliambulia patupu.

Hii ni baada ya kunyimwa tiketi ya ODM kuchuana na Johnson Sakaja aliyechaguliwa Gavana baada ya kumbwaga mpinzani wake Polycarp Igathe kwenye uchaguzi huo.

“Niko tayari kuhudumia Bungoma. Niko tayari kuwa rubani. Bungoma iko tayari kupaa,” alisema Wanyonyi anayepania kumrithi Gavana Ken Lusaka.

Lusaka haruhusiwi kugombea tena wadhifa huo kwani atakuwa amehudumu mihula miwili inayokubalika kisheria wakati wa kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa pia ni miongoni mwa wanaomezea mate wadhifa huo.

Share This Article