Netflix yashtakiwa kwa matatizo wakati wa pigano la Mike Tyson na Jake Paul

Marion Bosire
2 Min Read

Kampuni ya Netflix inayohusika na maonyesho ya video imeshtakiwa katika mahakama moja ya Tampa, Florida nchini Marekani na mmoja wa watumiaji wa jukwaa hilo.

Mlalamishi Ronald “Blue” Denton mkazi wa jimbo la Hillsborough katika kesi hiyo anadai kwamba Netflix ilikiuka mkataba na watazamaji na kutekeleza matendo yasiyo ya haki.

Kulingana naye, kosa hilo lilitendeka pale ambapo maonyesho ya moja kwa moja ya pigano la Mike Tyson na Jake Paul yalikumbwa na matatizo.

Denton anaelezea kwamba wamarekani wapatao milioni 60 walikuwa wanasubiri kwa hamu kutazama pigano hilo lakini wakakumbana na maonyesho mabaya.

Alitaja malalamishi yapatayo laki moja mitandaoni kuhusu ubora wa maonyesho hayo. Wapo waliodai kutoweza kupata jukwaa na Netflix wakati wa maonyesho hayo, maonyesho kukumbwa na hitilafu na muda mrefu wa kuanza kuonyesha baada ya kukwama.

Kulingana na tovuti ya Downdetector, inayofuatilia matatizo ya kimtandao watu wapatao elfu 98, waliripoti kukosa jukwaa la Netflix Ijumaa usiku, wakati wa maonyesho ya pigano hilo la kihistoria.

Wengine walisema kwamba Netflix ilipotea kabla ya kuanza kwa pigano na wengine wakalalamikia sauti na picha mbovu.

Kampuni ya Most Valuable Promotions ambayo ilikuwa inatangaza pigano la Tyson na Paul iliripoti kwamba watu milioni 60 walitizama pigano hilo mubashara kwenye Netflix.

Netflix na Most Valuable zilitaja maonyesho hayo ya moja kwa moja kama yaliyofanikiwa lakini mlalamishi katika kesi hii anasema watumiaji wa Netflix hawakupata walichotarajia kwani walikosa sehemu kubwa ya onyesho.

Kesi hiyo inakubalia walalamishi wengine kujiunga nayo na inasubiriwa kuona iwapo wengine watajitokeza.

Share This Article