Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atazuru Marekani Jumatatu, ziara ambayo wadadisi wanatumai itaangazia kusherehekea ushindi wa Marekani dhidi ya Iran na majadiliano kuhusu kukomesha vita vya Israel huko Gaza.
Hii ni mara ya tatu Netanyahu atakuwa anakutana na Rais Donald Trump, ambaye anasema Marekani na Israel ziliharibu kabisa vituo vya kinyuklia vya Iran katika makabiliano ya siku 12.
Wiki iliyopita, Trump alisema Israel imekubali masharti ya mpango wa kusitisha mashambulizi Gaza kwa siku 60, ili kutoa fursa kwa wahusika kujadili mwisho wa vita ambavyo vimedumu miezi 21.
Julai 4, 2025 kundi la Hamas lilikubali pendekezo la wapatanishi wa Qatar na Misri kuhusu kusitisha mapigano na Rais Trump akasema kwamba kutakuwa na maafikiano kufikia wiki ijayo.
Israel hata hivyo imesema kwamba Hamas wameomba mabadiliko kadhaa yafanywe kwenye masharti ya pendekezo la kusitisha mapigano lakini wawakilishi wa Israel hawakuridhia na leo wanaelekea Qatar kujadili pendekezo husika.
Watu wapatao elfu 57 wameuawa katika vita vya Israel huko Gaza kufikia sasa, wengi wakiwa wanawake na watoto. Wasomi wa sheria wa umoja wa mataifa wametaja hali hiyo kuwa mauaji ya halakiki dhidi ya Wapalestina.
Wajuzi hao hawana matumaini kwamba kusitisha vita hivyo kwa muda kutafungua njia ya kuvimaliza kabisa, wakiamini kwamba nia ya Rais Trump ni kuhakikisha kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel tu.