Netanyahu asema hakutakuwa na taifa la Palestina

Marion Bosire
2 Min Read
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kwamba hakutakuwa na taifa la Palestina huku akitia saini makubaliano ya kuendeleza mpango wa makazi utakaogawanya eneo la West Bank mara mbili.

Hatua hii ya Netanyahu inazima kabisa matumaini ya kuwepo kwa taifa la Palestina siku za usoni.

Kiongozi huyo wa Israel alitia saini makubaliano hayo jana Alhamisi ili kutoa idhini ya kuendelea kwa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la West Bank.

“Tutatimiza ahadi yetu kwamba hakutakuwa na taifa la Palestina. Eneo hili ni letu” alisema Netanyahu katika hafla moja katika eneo la Maale Adumim, makazi ya Wa-Israeli mashariki mwa Jerusalem.

Aliongeza kusema kwamba wataongeza hadi mara mbili idadi ya wakazi wa eneo hilo la ukubwa wa kilomita 12 mraba mashariki mwa Jerusalem lililopatiwa jina la ‘East 1’ au ‘E1’.

Mradi huo unajumuisha nyumba 3,400 mpya za wakazi wa asili ya Israel na utakata eneo kubwa la West Bank kutoka kwa eneo la Jerusalem mashariki ambalo tayari lina wakazi.

Eneo la Jerusalem Mashariki lina Wa-Palestina wengi ambao kwa muda mrefu wamekuwa na matumaini kwamba huo utakuwa mji mkuu wa litakalokuwa taifa la Palesina.

Maeneo ya makazi ya Wa-Israeli huko West Bank, ambayo yamekaliwa tangu mwaka 1967, yanachukuliwa kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa hata ingawa kuna idhini ya Israel.

Huku haya yakijiri, msemaji wa mamlaka ya Urais wa Palestina Nabil Abu Rudeineh amesisitiza kwamba taifa la Palestina ambalo jiji lake kuu litakuwa East Jerusalem ni muhimu kwa amani ya eneo hilo.

Share This Article