Mataifa ya Bara Afrika, yamehimizwa kuongeza ufadhili katika sekta Kilimo, ili kuhakikisha utoshelevu wa chakula na maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza leo Alhamisi wakati wa siku ya mwisho ya kongamano kuhusu ufadhili endelevu wa mifumo ya kilimo kuhusu uzalishaji chakula, FINAS 2025 jijini Nairobi, waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi alisema, wakulima wadogo wadogo barani humu, wanakumbwa na changamoto kubwa za ukosefu wa ufadhili kuendeleza kilimo chao.
“Hatuhitaji ufadhili tu, tunahitaji ufadhili bora,” alisema Mudavadi.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje, aidha alidokeza kuwa wakulima wengi wameshindwa kufikia soko la bidhaa zao, wanakabiliwa na changamoto za bei na pembejeo za kilimo kama vile mbegu zilizoidhinishwa, mbolea na vifaa vya kilimo.

Alitoa wito wa kutathminiwa upya kwa mfumo wa ufadhili wa kilimo barani humu, akisema miundo ya awali imeshindwa kuleta mabadiliko yanayohitajika.
Mudavadi alikariri haja ya uwekezaji thabiti katika muundo msingi, teknolojia ya kilimo, utafiti na uptikanaji jumuishi wa fedha.
Kongamano la FINAS 2025, liliwaleta pamoja washiriki wa aina mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wabunifu wa kidijitali, wadau wa sekta ya kibinafsi na waakilishi wa serikali ya kitaifa na kanda.