Nchi ya Cyprus yafungua ubalozi wake Jijini Nairobi

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi na mwenzake wa Cyprus Dkt. Constantinos Kombos, wakifungua ubalozi wa Cyprus Jijini Nairobi.

Nchi ya Cyprus imefungua ubalozi wake jijini Nairobi,  katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi na mwenzake wa Cyprus Dkt. Constantinos Kombos.

Mudavadi alisema ufunguzi wa ubalozi huo Nairobi, utapiga jeki uhusiano wa nchi hizo mbili kwa kuweka msingi thabiti wa ushiriliano na majadiliano.

“Ufunguzi huu utabuni nafasi zaidi kwa ukuaji wa uchumi, kukabiliana na changamoto zilizopo na kufanikisha uunganishaji wa watu wa mataifa hayo,”alisema Mudavadi.

Kwa upande wake waziri Kombos, alisifu Kenya kwa kuwa na mazingira bora yanayovutia na kupiga jeki mabalozi, akidokeza kuwa Nairobi inazidi kuwa kitovu cha diplomasia na shughuli za biashara.

Aidha alihakikishia Kenya kwamba Cyprus itaunga mkono utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi  baina ya Kenya na Jumuiya ya Ulaya, litakapotwaa urais wa Baraza la Jumuiya hiyo mwaka ujao.

“Tunatazamia kuwa uhusiano huu utakuwa na manufaa kwa raia wetu na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili,”alisema Kombos.

Kenya na Cyprus zimeafikiana kuimarisha uhusiano katika nyanja za uchumi wa majini, ubaharia na uchukuzi wa majini ambao ni muhimu katika kuimarisha sekta ya utalii.

Share This Article