Abiria 60 na wafanyakazi wanne walikuwa ndani ya ndege iliyoanguka katika mto wa Potomac karibu na uwanja wa ndege wa Ronald Reagan Washington viungani mwa mji mkuu wa Marekani, kwa mujibu wa shirika la habari la NBC NEWS.
Ndege hiyo ilianguka baada ya kugongana angani na helikopta ya jeshi la Marekani.
Mamlaka ya Usimamizi wa Anga, FAA katika taarifa imesema ndege hiyo iligongana na helikopta hiyo wakati ikikaribia kutua kwenye barabara ya ndege majira ya saa tatu usiku jana Jumatano, kwa saa za eneo hilo.
Ndege hiyo ilikuwa ikitokea Wichita, Kansas wakati wa ajali hiyo.
Kulingana na FAA, ndege hiyo ilikuwa ya shirika la ndege la American Airlines yenye nambari ya usajili 5342, aina ya Bombadier CRJ700.
Ndege hiyo imeripotiwa kuwa na uwezo wa kubeba watu 70.
Polisi jijini Washington wameripotiwa wakisema polisi na taasisi kadhaa kwa sasa zinafanya uratibu wa shughuli ya utafutaji na uokozi katika mto huo.
Ndege zote zimezuiwa kutoka na kutua katika uwanja huo.