Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Nazizi, ametoa wimbo mpya unaoitwa “Gai Fafa” ulioandaliwa na marehemu Hilton Mwakio, anayefahamika pia kama ‘Herbalist’.
“Gai Fafa” ni wimbo wa kuinua moyo unaohamasisha kuhusu kuachilia mizigo ya maisha na kuchagua kusherehekea.Nazizi anauona wimbo huu kama zawadi kwa mashabiki wake na heshima kwa rafiki aliyempenda sana.
“Wimbo huu ni kwa ajili ya mashabiki ambao wamekuwa nami kwa miaka 25, hasa katika kipindi kigumu cha huzuni nilichopitia hivi karibuni,” alisema Nazizi.
Aliongeza kwamba hana namna ya kuelezea jinsi jumbe za mashabiki hao na maneno ya faraja vilikuwa na maana kubwa kwake.
“Nilihitaji kusema asante kwa njia ninayoijua vyema – kupitia muziki. Na wimbo huu pia ni kwa ajili ya Hilton. Aliupenda sana na alikuwa akinisisitiza niutoe. Huu ni wake pia.” alisema Nazizi.
Video ya wimbo huo “Gai Fafa” ilirekodiwa huko Arusha, Tanzania chini ya uongozi wa mwelekezi kwa jina Okey na wacheza densi wake wanaojiita Purple Dancers Crew.
Wakufunzi wa densi Chiki na Kevo kutoka The Dance Shagz nchini Kenya pia walihusika.
Wimbo huu uliimbwa kwa mara ya kwanza hadharani kwenye tamasha la Blankets & Wine mwezi Desemba 2024, ambapo Nazizi aliuliza umati iwapo anaweza kuutoa rasmi – na shangwe za mashabiki zikampa kibali.
Akitambulika kama First Lady wa reggae na hip hop ya Kenya, Nazizi ameleta hisia za furaha na uhuru kupitia wimbo huu mpya.
“Unahusu kuachilia msongo, kucheza kwa moyo wote na kuruhusu nafsi yako kufurahia, hata kama ni kwa muda mfupi. Hii ndiyo video yangu ya kwanza kabisa inayojikita kwenye dansi na ninasubiri kwa hamu kuona video za mashidano ya densi zitakazochapishwa mitandaoni.”
Nazizi anajitahidi pia kuzindua EP ya reggae yenye nyimbo sita baadaye mwaka huu kwa ajili ya mashabiki wake wa reggae.
Msanii huyo wa hip hop na reggae ni nguvu kubwa katika tasnia ya muziki wa Kenya na Afrika na ametambuliwa na taasisi andalizi ya tuzo za Grammy almaarufu The Recording Academy kama mmoja wa wanamuziki wa kike wa mtindo wa rap Afrika walioweka msingi wa muziki huo.