Navio ashauri wanamuziki wenza kuangazia sanaa

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa mtindo wa Hip hop nchini Uganda Daniel Lubwama Kigozi maarufu kama Navio, ana ushauri kwa wanamuziki wenzake katika mtindo huo wa kufoka foka.

Kulingana naye uthabiti ni muhimi kwa yeyote ambaye angependa kufurahikia taaluma yenye ufanisi katika muziki wa Rap.

Navio anafahamika kwa muziki wake mzuri unaopendwa ndani na nje ya Uganda ambao amekuwa akipakulia mashabiki zake kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Msanii huyo ameweza kusalia imara katika kitengo hicho cha muziki ambacho ni kigumu kwani hakipendelewi sana na mashabiki.

Anapojiandaa kwa tamasha lake la kwanza kabisa msanii huyo anasema kwamba uthabiti na kuangazia sanaa yake ndivyo vimekuwa vitu vya maana katika kazi yake.

“Kwetu sisi wasanii wa muziki wa rap, funzo liko wazi: angazia sanaa” alisema Navio katika mahojiano akisema kwamba wasanii ambao walijaribu kuangazia mambo mengine waliisha.

Kulingana naye, muziki huo umebadilika kutoka tu kuwa talanta na sasa unahusu ukuaji, mabadiliko na kukubali hali ilivyo sasa.

Navio alianza kazi kama mwanamuziki mwaka 200 wakati huo akiwa mwanachama wa kundi la Klear Kut, akiwa na wenzake The Mith na JB. Kundi hilo ndilo lilianzisha “Ugaflow” jina linalorejelea hip hop ya Uganda.

Kando na kuwa mwanamuziki, Navio pia anajihusisha na shughuli za kurekodi muziki kupitia kwa kampuni yake iitwayo NavCorp.

Share This Article