Klabu ya Nairobi United ndio mabingwa wa Ligi ya daraja ya kwanza humu nchini (NSL), msimu wa mwaka 2024/2025.
Hii ni baada ya kusajili ushindi wa bao moja kwa bila Jumamosi alasiri dhidi ya MOFA katika mchuano wa raundi ya 34.
Nairobi United wanaongoza jedwali kwa pointi 72 baada ya mechi 34, huku wakitarajiwa kufunga msimu wikendi ijayo dhidi ya Naivas FC.
Timu hiyo inayofadhiliwa na serikali ya kaunti ya Nairobi itashiriki Ligi Kuu ya FKF, msimu ujao pamoja na Administration Police Service Bomet FC, ambao wamejihakikishia nafasi ya pili.
Aidha kivumbi kinatarajiwa katika mechi ya mwisho huku timu tatu za Naivas FC,Darajani Gogo na Fortune Sacco.
Darajani Gogo walio na alama 59, kufuatia ushindi wa leo wa mabao 2-1 dhidi ya Fortune Sacco, watafunga msimu nyumbani dhidi ya Luanda Villa .
Upande mwingine Naivas FC, walio na alama sawa 59, watakamilisha msimu dhidi ya mabingwa Nairobi United, huku Fortune Sacco, yenye pointi 57, ikifunga kazi ugenini dhidi ya Kisumu All Stars.
Timu itakayomaliza nafasi ya tatu itachuana na timu nambari 16 katika Ligi Kuu ya FKF kuwania kupandishwa daraja kushiriki Ligi Kuu.