Nairobi Hospital yasitisha nyongeza ya malipo ya matibabu

Tom Mathinji
1 Min Read
Nairobi Hospital yabatilisha nyongeza ya ada za matibabu.

Nairobi Hospital imebatilisha utekelezaji wa nyongeza ya ada za matibabu kwa asilimia tano, jinsi ilivyokuwa imetangaza hapo awali.

Kupitia kwa taarifa Ijumaa usiku, hospitali hiyo ilisema hatua hiyo iliafikiwa baada ya mashauriano ya kina na kampuni za bima, ambazo zilikuwa zimesitisha huduma zao katika hospitali hiyo.

“Usimamizi wa hospitali hii ulishiriki meza ya mazungumzo na wawakilishi wa kampuni za bima Agosti 11, 2025….Hospitali hii ingependa kuwafahamisha kwamba ada za matibabu zitasalia jinsi zilivyokuwa,” ilisema taarifa ya hospitali hiyo.

Hospitali hiyo ilisema sasa iko tayari kushirikiana na kampuni za bima, kuhakikisha huduma bora kwa wateja.

“Tunahakikishia umma kwamba tutaendelea kutoa huduma za ubora wa hali ya juu kwa wateja wetu,” iliongeza taarifa hiyo.

Kampuni za bima hapo awali zilikuwa zimesimamisha huduma kwa muda katika hospitali hiyo, kutokana na gharama ya juu ya matibabu iliyotokana na marekebisho ya muda mfupi ya viwango vya malipo hospitalini humo.

Taarifa ya kusitishwa kwa huduma hizo ilitolewa kwa wateja mapema mwezi huu, na kuzua wasiwasi miongoni mwa wagonjwa na wafanyakazi wa matibabu, huku baadhi ya familia zikiripotiwa kutafuta huduma kwenye vituo vingine vya afya.

Share This Article