Nairobi City Thunder yapoteza mechi ya tatu mtawalia

Tom Mathinji
2 Min Read
Timu ya City Thunder katika mashindano ya mpira wa kikapu kanda ya Nile.

Nairobi City Thunder ilipoteza mechi yake ya tatu mtawalia ya ligi ya mpira wa kikapu barani Afrika kanda ya Nile baada ya kushindwa alama  75-74 na MBB ya Afrika Kusini katika uwanja wa ndani wa BK ,jijini Kigali, Rwanda.

MBB ilishinda robo ya kwanza vikapu 22-15 lakini Thunder  iliyoongozwa na mchezaji mahiri Tylor Ongwae ilijizatiti na kushinda robo ya pili  18-10 na kuongoza kwa vikapu 33-32 ilipofikia wakati wa mapumziko.

Thunder iliendeleza umahiri wake katika kipindi cha tatu ilichotwaa pointi 27-18, Lakini MBB ilirejea mchezoni katika robo ya nne na kuifunga Thunder vikapu 25-14 na kupata ushindi,japo finyu wa alama   75-74.

Ushindi huo ulikuwa ni wa kwanza wa MBB kati ya mechi tatu iliyocheza  katika mashindano hayo ya   BAL ilhali Thunder inayoongozwa na kocha mkuu  Bradley Ibs haijashinda mechi yoyote katika mashindano hayo yanayooandaliwa kwa mfumo wa ligi.

Ushinde unaiwacha Thunder  na kazi ngumu ya kushinda michuano yake mitatu iliyosalia ili ifufue matumaini ya kufuzu fainali ya ligi hiyo mwezi ujao jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Thunder itamenyana na  Al Ahli Tripoli alhamisi  kabla ya kucheza na MBB jumamosi kisha ihitimishe michuano hiyo dhidi ya wenyeji APR jumapili.Timu mbili za mwanzo zitafuzu fainali hizo za Ligi ya mpira wa kikapu jijini Pretoria mwezi ujao.

Share This Article