Naibu Kamishna Mkuu wa Magereza, wengine 4 washtakiwa kwa ulaghai

Martin Mwanje
1 Min Read

Naibu Kamishna Mkuu wa Magereza Benjamin Obuya na watu wengine wanne leo Jumatatu wameshtakiwa katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani. 

Watano hao wameshtakiwa kwa madai ya kujipatia shilingi milioni 302 kama malipo kwa bidhaa ambazo kamwe hazikuwasilishwa.

Obuya, na wafanyakazi wenzake wa Idara ya Magereza Joseph Kamau (Mhasibu Mkuu), James Nyang’au Gekobe (Mhasibu II), Joseph Ochoki Omaiyo (Mlinzi) na mafanyabashara Steven Kisonzo Mulwa, wanatuhumiwa kwa kula njama ya kutekeleza uhalifu wa kiuchumi.

Mashtaka dhidi yao yanaelezea kuwa kati ya Julai 1, 2014 na Machi 29, 2018, walijipatia mali ya umma yenye thamani ya shilingi milioni 301.9 kwa madai ya kuwaslisha bidhaa kwa Idara ya Magereza ambazo kamwe hazikuwasilishwa.

Aidha, wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia vibaya mamlaka yao, kujipatia mali ya umma kwa ulaghai na ulanguzi wa fedha.

Wote hao walikanusha mashtaka dhid yao walipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Celesa Asis Okore na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 7 na mdhamini wa kiasi sawia cha fedha au dhamana ya pesa taslimu ya shilingi milioni 4. Wametakiwa kusalimisha pasipoti zao mahakamani.

Kesi dhidi yao itatajwa Agosti 2, 2024.

Share This Article