Wale wote wanaotaka kuwa makamishna wa Tume huru ya Uchaguzi na uratibu wa Mipaka nchini IEBC, sasa wana fursa ya kutuma maombi yao kuanzia Februari 1, 2025.
Hii ni baada ya Jopo la watu tisa lililobuniwa kuwateua makamishna pamoja na mwenye kiti wa tume ya IEBC, kusema kuwa litatangaza nafasi ya mweyekiti na makamishna wa IEBC Jumamosi na kukaribisha maombi kutoka kwa wakenya ambao wamehitumu kwa nyadhifa hizo.
“Mnamo Jumamosi Februari 1, 2025, Jopo hili litakaribisha maombi kutoka kwa wakenya kwa wadhifa wa myenyekiti na makamishna wa tume ya IEBC,” ilisema taarifa ya tume hiyo.
Jopo hilo ambalo lilibuniwa rasmi siku ya Ijumaa baada ya kuapishwa kwa wanachama wawili waliosalia, Fatuma Saman na Carolene Kituku, limeanza kutekeleza rasmi majukumu yake, huku shughuli ya kwanza ikiwa ni kumchagua mwenyekiti wake na naibu mwenyekiti.
Dkt. Nelson Makanda alichaguliwa mwenyekiti wa jopo hilo, naye Lindah Kiome akiwa naibu mwenyekiti.
Makanda alihakikishia umma kuwa jopo hilo linalenga kuwateua makamishna na mwenyekiti wa IEBC, katika muda wa miezi mitatu ijayo.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa Wakenya ambao wamehitimu kwa nyadhifa hizo kutuma maombi yao, akisema zoezi hilo litatekelezwa kwa usawa.
“Nawahakikishia wakenya kwamba jopo hili limejitolea kutekeleza zoezi hilo kwa uwazi na usawa,” alisema Dkt. Makanda.