Nadia Mukami asema hapendi kazi ya kuandaa video za muziki

Kulingana naye, kazi hiyo inahusisha mengi na inaweza kuchukua muda mrefu.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Kenya Nadia Mukami amesema kwamba hapendi kazi za kuandaa video za muziki akitaja kazi nyingi na msongo wa mawazo.

Kupitia Instagram msanii huyo aligusia matukio ya awali yaliyotokea wakati wa maandalizi ya video kama hizo ili kuunga mkono usemi wake.

Tukio la hivi karibuni zaidi ni la maandalizi ya video ya wimbo uitwao Overdose ambao amehusisha msanii Bensoul ambapo mvua kubwa ilinyesha na walikuwa wafanye kazi hiyo nje.

Anasema mvua ilikoma kwa muda wa saa moja na walilazimika kuharakisha pakubwa kunakili video katika eneo hilo kabla ya mvua kuanza kunyesha tena.

Walipoelekea katika eneo jingine la kuandaa kazi hiyo, mvua iliwafungia kwa masaa matatu na ilipokoma wakafanya kazi yao na walikuwa wakienda kwenye eneo la tatu saa saba usiku, siku hiyo walifika nyumbani saa moja asubuhi.

Katika tukio jingine anasema alipata ajali mbaya wakati wa maandalizi ya video ya wimbo “Siko sure” huku mmoja wa wahusika wa maandalizi hayo naye akipata ajali na kuishia kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Walilazimika kufutilia mbali kazi hiyo.

“Video ya wimbo KIPEPEO tulilazimika kuandaa video upya kwani hatukuwianisha ya awali na maneno ya wimbo” aliandika Nadia akisema kwamba hatua hiyo ilimgharimu fedha zaidi.

Msanii huyo alielezea kwamba maandalizi ya video sio kazi rahisi na wakati mwingine huchukua hata siku kadhaa kabla ya kuafikia lengo.

Huku haya yakijiri, msanii huyo ambaye amefichua hivi maajuzi kwamba anatarajia mtoto wake wa pili amesema kwamba video ya “Overdose” itatoka Ijumaa.

Share This Article