NACADA yatangaza washindi wa shindano la uandishi wa insha

Martin Mwanje
2 Min Read
Wanafunzi wanaoishi na ulemavu pia walishiriki shindano la uandishi wa insha

Mamlaka ya Taifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Mihadarati (NACADA) imetangaza washindi wa shindano la taifa la uandishi wa insha katika shule za upili.

Shindano hilo lililenga kuwahusisha wanafunzi katika mazungumzo muhimu ya kuzuia matumizi ya mihadarati nchini.

Shindano hilo lilihusisha washiriki 410 kutoka kaunti 30, ambapo wasichana  301 na wavulana 109 waliwasilisha insha zao kuhusu mada mbalimbali juu ya kuzuia matumizi ya pombe na mihadarati.

Katika uandishi wa insha hizo, wanafunzi walipewa fura ya kuelezea matumizi ya mihadarati shuleni na namna ya kuyapiga dafrau.

Ivanka Blessing Odera kutoka shule ya wasichana ya Moi Girls Isinya aliibuka mshindi wa jumla katika kipengele cha uandishi wa insha kwa lugha ya Kiingereza huku Vallary Racheal kutoka shule ya wasichana ya St. Mary’s Mumias na Wesley Lambaric Mmbaya kutoka shule ya Njiiri wakishikilia nafasi za pili na tatu mtawalia.

Katika kipengele cha uandishi wa insha katika lugha ya Kiswahili, Rhoda Kanoti kutoka shule ya wasichana ya St. Mary’s Igoji aliibuka kidedea akifuatwa na Maryanne Wangeci Wambugu kutoka shule ya sekondari ya wasichana ya Birithia na Joy Chepchumba kutoka shule ya upili ya wasichana ya Kipsigis mtawalia.

Shindano hilo pia lilihusisha kipengele maalum cha wanafunzi wanaoishi na ulemavu.

Katika kipengele hicho, Odiero Dancan Ochieng kutoka shule ya upili maalum ya Joyland kutoka kaunti ya Kisumu aliibuka mshindi huku Okumu Sarah Mical akiibuka wa pili.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA Dkt. Anthony Omerikwa aliwapongeza washiriki kutokana na insha zao zilizokuwa na mapendekezo maridhawa na kuelezea hatua hiyo kuwa ushuhuda tosha wa namna vijana wanavyoweza kuchochea mabadiliko nchini.

“Vijana hawa wameandika insha zinazotoa changamoto kwa hali za kawaida, zinazohamasisha kuchukuliwa kwa hatua na kuelezea matumaini ya Kenya isiyokuwa na matumizi ya dawa za kulevya. Ubunifu na kujitolea kwao ni nguvu, na kwamba vijana ni muhimu katika kufikia jamii yenye afya nzuri na iliyo salama,” alisema Dkt. Omerikwa.

 

TAGGED:
Share This Article