Mbunge wa eneo la Matungu lililo katika kaunti ya Kakamega Peter Nabulindo ametishia kuondoka kwenye chama cha upinzani ODM.
Kiongozi huyo alikuwa akihutubia watu wa eneo lake leo ambapo alisema iwapo chama hicho kitakoma kushirikiana na serikali ya Rais William Ruto, basi ataondoka.
Kulingana naye, marehemu waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, aliacha chama hicho kikiwa kwenye serikali jumuishi na majaribio yoyote ya viongozi wa chama hicho kukiondoa huko yatasababisha agure.
Nabulindo aliwanyoshea kidole cha lawama, wanachama fulani wa ODM ambao anasema wanachochea maandamano kote nchini dhidi ya serikali akionya kwamba matendo kama hayo hayastahili.
Mbunge huyo alishangaa kilichochochea miito ya maandamano akisisitiza kwamba serikali ya sasa imeafikia mengi katika muda wa chini ya miaka mitatu pekee akitaja nyumba za gharama nafuu na uunganishaji umeme.
“Tutasalia kwenye serikali jumuishi na iwapo viongozi wa Nyanza watajaribu kwenda barabarani, basi tutawaachia ODM na kuunga mkono serikali ya Rais Ruto” alisisitiza Nabulindo.
Matamshi ya Nabulindo yanajiri wakati ambapo kumekuwa na mvutano na chuki fulani katika chama cha ODM huku baadhi ya wanachama wakionekana kutoridhishwa na uhusiano wa chama hicho na serikali ya sasa.
Babu Owino mbunge wa Embakasi mashariki ameonya kuhusu uwezekano wa kusambaratika kwa ODM iwapo itaendelea kushirikiana na Rais.
Gavana wa Siaya James Orengo naye anatilia shaka yaliyomo kwenye mkataba wa maelewano uliotiwa saini kati ya ODM na UDA mwaka jana.