Mwimbaji Taarab Mwapombe Hiyari afariki

Bi. Mwapombe alifariki usiku wa kuamkia jana Jumanne Februari 11, 2025.

Marion Bosire
2 Min Read
Bi. Mwapombe na Rais Hussein Mwinyi

Taifa la Tanzania linaomboleza kifo cha mwimbaji mkongwe wa muziki wa Taarab Bi. Mwapombe Hiyari.

Kifo chake kilitangazwa na Baraza la Sanaa la Taifa – BASATA lililofafanua kwamba alifariki usiku wa kuamkia jana Jumanne Februari 11, 2025.

“Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linasikitika kutangaza kifo cha mwimbaji mkongwe wa taarab kutoka Zanzibar, Bi. Mwapombe Hiyari, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Jumanne, 11 Februari 2025.” Ilianza taarifa hiyo ya BASATA

Bi. Mwapombe Hiyari atakumbukwa kama gwiji wa taarab aliyeweka alama isiyofutika katika historia ya muziki wa mwambao, kulingana na BASATA.

Baraza hilo liliongeza kusema kwamba Kupitia sauti yake nyororo na uimbaji wake wenye hisia, aliwahi kushirikiana na mabingwa wa taarab kama Sammi Hadji Dau na baadaye Abeid Bakari katika wimbo wake maarufu Sabalkheri Mpenzi, uliopendwa na vizazi mbalimbali.

BASATA ilitoa pole kwa familia yake, ndugu, marafiki na wadau wa sanaa kwa msiba huo mkubwa.

“Tunatambua mchango wake adhimu katika kuendeleza na kuhifadhi urithi wa muziki wa taarab. Roho yake ilazwe mahali pema, na urithi wake wa muziki uendelee kuishi milele.” ilisema BASATA.

Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi amemwomboleza Mwapombe na kumtaja kuwa mwimbaji bingwa aliyewika enzi za uhai wake.

Amesema Zanzibar imepoteza mmoja kati ya wasanii nyota waliowika ndani na nje ya Zanzibar na kuipatia sifa kemkem.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kifo cha Msanii huyo hodari ni pigo kubwa katika fani ya Taarab Zanzibar huku akiwatumia salamu za pole ndugu, jamaa, marafiki, familia na wanachi wote wa Tanzania na Zanzibar.

Share This Article