Mwimbaji wa nyimbo za injili Beatrice Wairimu Mbugua maarufu kama Betty Bayo amefariki akiendelea kupokea matibabu katika hospitali kuu ya Kenyatta.
Jumbe kuhusu kifo chake zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia asubuhi leo, huku watu maarufu hasa katika tasnia ya muziki wa injili wakichapisha jumbe za kumwomboleza.
Daddy Owen aliandika, “Lala kwa amani mmoja wetu Betty Bayo. Nyoyo zetu zimevunjika na kifo hiki. Betty alikuwa zaidi ya sauti tu katika tasnia ya nyimbo za injili, alikuwa chombo cha neema.”
Aliendelea kumsifia kutokana na jinsi alijitolea katika kueneza injili kupitia nyimbo zake, upole wake na imani ambayo iligusa wengi. Owen alitoa pole zake kwa ndugu jamaa na marafiki wa Betty Bayo huku akiwatakia faraja kutoka kwa mwenyezi Mungu.
“Mbingu kwa kweli zimefaidi kwa kupata mtu aneyejua kuabudu. Pumzika salama Betty. Umemaliza mwendo wako kwa imani na upendo.” alimalizia Daddy Owen.
Mhubiri Ben Kamau Kiengei katika ujumbe wake alifichua kwamba Betty alikuwa akiugua ugonjwa wa saratani ya damu almaarufu “Leukemia” ambao uligunduliwa hivi maajuzi ukiwa tayari umefika kiwango cha juu.
Mchekeshaji Njugush alichapisha picha ya Betty Bayo kwenye Instagram na kuandika, “Maisha ni mafupi sana!!! Lala salama Betty Bayo huku mwenzake Mamito Eunice akiandika, “Aliimba nyimbo nzuri ambazo zilitupa matumaimi! Ameenda mapema sana! Pole kwa familia.”
Betty Bayo alijulikana sana kwa kuimba nyimbo za injili kwa lugha ya Gikuyu na ameacha watoto wawili aliojaliwa na aliyekuwa mume wake mhubiri Victor Kanyari.