Mwili wa mpiga gitaa na mwanamuziki wa mtindo wa Soukous wa asili ya DR Congo umezikwa leo katika makaburi ya Gombe jijini Kinshasa, nchini Congo.
Maziko hayo yaliandaliwa baada ya ibada ya wafu iliyoandaliwa mapema leo Machi 6, 2025, katika kanisa katoliki la Our Lady of the Congo lililoko Lingwala, jijini Kinshasha.
Mwili huo wa Papa Noel uliwasili katika uwanja wa ndege wa Nd’jili jijini Kinshasa Machi 4, 2025 saa mbili usiku.
Mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Antoine Nedule Monswet, alizaliwa Disemba 29, 1940 jijini Kinshasa na akafariki Novemba 11, 2024 nchini Ufaransa.
Awali wengi waliamini kwamba alizaliwa tarehe 25 mwezi Disemba ndiposa akapatiwa jina la Noel, lakini baadaye mke wake aliwakosoa akisema tarehe halisi ya kuzaliwa kwake ni Disemba 29.
Nedule aliwahi kuwa mwanachama wa bendi ya TPOK Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na François Luambo Makiadi, na ambayo ilitawala tasnia ya muziki nchini Congo kuanzia miaka ya 1950 hadi miaka ya 1980.
Baadaye alijiunga na bendi ya Kekele iliyobuniwa mwaka 2000 na akawa kiongozi wake, lakini ugonjwa ulimfanya akose kuhudhuria mikutano ya kurekodi nyimbo na ziara za kikazi.