Mwili wa Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki, jimbo la Kakamega, marehemu Phili Sulumeti, umewasili katika Parokia Kuu ya Jimbo la Kakamega leo Alhamisi usubuhi.
Awali, mwili huo ulibebwa kwa ndege kutoka jijini Nairobi hadi Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kisumu ambapo ulilakiwa na kubarikiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kisumu Maurice Muhatia Makumba pamoja na mapadri, viongozi na wakiristo wengi wa kanisa hilo.
Baada ya kuwasili, waumini walipewa fursa ya kuutazama mwili kwa heshima ya mwisho huku wengi wakibubujikwa na machozi.
Baadaye leo na usiku kucha, misa lukuki za kumuenzi na kubariki roho yake zitaandaliwa huku waumini wengi wakitarajiwa kuhudhuria.
Kwa mujibu wa ratiba, kutaandaliwa maombi ( Vespers ) saa 11:30 leo jioni kisha 12:00, Jimbo la Bungoma lifungue ukurasa wa misa hizo takatifu likifuatwa na Dinari za Mumias, Chekalini, Eregi na Mukumu. Saa 3:00 itakuwa Misa ya mapadri na makundi teule. Mwisho itakuwa Dinari ya Kakamega hiyo kesho, saa 11:00 alfajiri.
Hapo kesho Ijumaa, misa ya wafu itafanyika ugani Bukhungu na inatarajiwa kuhudhuriwa na halaiki ya wakristo wa dhehebu hilo na madhehebu mengine, viongozi wa serikali kuu na kaunti, wanasiasa na wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali.
Hatimaye, mwili utazikwa katika kanisa la parokia kuu ya jimbo hilo.