Mwigizaji wa mitandaoni Mr KK Mwenyewe afariki

Alifariki katika hospitali ya Kiambu Level 4 ambapo alikuwa amelazwa akipokea matibabu.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji wa mitandaoni Zachariah Kariuki ambaye wengi wanamfahamu kama KK Mwenyewe amefariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.

KK alijulikana na wengi kufuatia video zake za kumwigiza aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kifo chake kilitokea jana Jumatatu usiku katika hospitali ya Kiambu Level 4 ambapo alikuwa akipokea matibabu.

Kafengo mwigizaji mwingine wa mitandaoni ambaye aliwahi kushirikiana na KK kwenye maigizo ndiye alitangaza habari hizo kwenye akaunti yake ta Tik Tok.

“Tunasikitika kutangaza kifo cha ghafla cha Zachariah Kariuki maarufu kama Mr. KK Mwenyewe. Aliaga dunia jana jioni akipokea matibabu katika hospitali ya Kiambu” aliandika Kafengo kwenye ujumbe huo aliochapisha leo alfajiri.

Kafengo aliomba mashabiki wa mwendazake usaidizi na maombi wakati huu wa majonzi huku akitakia familia ya Zacharia na marafiki faraja.

Hata hivyo Kafengo hakufichua mara moja ugonjwa uliokuwa ukimsibu KK na kusababisha kifo chake.

Share This Article