Mwigizaji maarufu nchini Bilal Wanjau amefariki,
Taarifa za kifo chake zilitolewa mtandaoni na mwigizaji mwenza Sandra Dacha aliyechapisha video ya pamoja wakifanya mzaha na Bilal.
“Kwa huzuni kubwa ninatangaza kifo cha ghafla cha mwenzangu Bilal mapema asubuhi ya leo kutokana na matatizo ya kisukari.” Aliandika Dacha akiongeza kwamba Bilal alikuwa msanii bora na mwenye kipaji cha kipekee.
Kulingana na Dacha, mwendazake atazikwa kesho Ijumaa Disemba 5, 2025 nyumbani kwao huko Machakos.
Dacha alidhihirisha huzuni akisema kama tasnia ya uigizaji wamepoteza mmoja wa waigizaji bora huku akihimiza umma uiombee familia ya Bilal.
Bilal Wanjau anafahamika kwa kuigiza kwenye vipindi kama Tahidi High, Gavana, Mjinga na Ushenzi,Sumu la Mapenzi na Jela. Ni mwana wa mwanandondi wa zamani Ibrahim “surf” Bilal, aliyewahi kushinda medali ya shaba kwenye olimpiki.
Uchu wake kwa uigizaji uliota akiwa mwanafunzi katika shule ya upili ya wavulana ya Mtakatifu Teresa na ukaendelea alipohamia shule ya upili ya Eastleigh.