Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNCHR ina mwenyekiti mpya.
Claris Awuor Ogangah alichukua uongozi wa tume hiyo leo Jumatatu baada ya kuapishwa katika halfa iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Ogangah anaziba pengo lililoachwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo Roselyn Odede.
Wengine walioapishwa ni John Cox Lorionokou kujaza pengo lililoachwa na Anne Nderitu kama Msajili wa Vyama vya Kisiasa.
Nderitu kwa sasa anahudumu kama kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.

Lorionokou atasaidiwa kwenye wadhifa huo na Agatha Wahome.

Aidha, Billy Komintai Konchelah ameapishwa kama mwanachama wa Baraza la Taifa la Mashujaa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Jaji Koome aliwataka wote hao kuheshimu siyo tu katiba bali pia Wakenya katika utendaji kazi wao.
“Afisi ya umma ni dhamana takatifu inayohitaji uadilifu, kutokuwa na upendeleo, na dhamira isiyoyumba ya kuhudumu kwa uaminifu na bidii,” alisema Jaji Mkuu.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK Faith Odhiambo amemtaka mwenyekiti mpya wa KNCHR kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za kibinadamu kama inavyohitajika kikatiba.
“Tuna imani kwamba uongozi wako utaongeza ari hiyo na kuipandisha hata juu zaidi. Tumikia kwa uadilifu,” Odhiambo alimshauri Ogangah.