Mwenyekiti mpya wa Baraza la Magavana (CoG) atabainika leo Jumatatu.
Wadhifa huo umekuwa ukishikiliwa na Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru ambaye amehudumu kwa kipindi cha mihula miwili baada ya kuchaguliwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 2022.
Wale wanaolenga kumrithi Waiguru ni Naibu Mwenyekiti wa sasa wa CoG ambaye pia ni Gavana wa Wajir Ahmed Abdulahi, Mutahi Kahiga (Nyeri), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi) na Joseph Ole Lenku (Kajiado).
Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja pia yupo kwenye orodha ya Magavana wanaotaka kuhudumu kama mwenyekiti wa CoG.
Uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa CoG na nyadhifa zingine kwenye baraza hilo utafanyika wakati wa mkutano wa Magavana hao unaofanyika katika hoteli moja jijini Nairobi.
Wakati wa mkutano huo, Magavana pia watapigia darubini Bima mpya ya Afya ya Jamii, SHIF na namna uzinduzi wake wiki jana ulivyoathiri utenda kazi wa serikali za kaunti.
Magavana wamekuwa wakitoa wito wa kuongezwa kwa mgao wa fedha za kaunti ili kuhakikisha utekelezaji wa bima hiyo hakumbani na visiki.