Maafisa wa polisi kaunti ndogo ya Magarini, kaunti ya Kilifi, wanachunguza kisa ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 25 alimuua babake mwenye umri wa miaka 80, kabla ya kuuawa na wananchi.
Ismail Karisa Mwaiha anadaiwa kukasirishwa na hatua ya babake ya kutompa ruhusa ya kuvuna maembe, na hapo mzozo ukaanza kabla ya mshukiwa huyo kumshambulia kwa shoka na kumkata babake mara kadhaa.
Watu wa familia hiyo waliokuwepo walipiga kamsa na kuvutia umati uliomshambulia mwanamume huyo kwa vifaa vya aina tofauti na kumuua papo hapo.
Kulingana na walioshuhudia, Ismail amekuwa akimdhulumu na kumtishia babake, na kwamba aliwahi fungwa gerezani kwa muda wa miaka miwili.
Kamanda wa polisi kaunti ya Kilifi Fatuma Hadi, aliyethibitisha kisa hicho, alisema polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha mauaji hayo mawili, akionya kuwa watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua za kisheria.
Huku akilaani mauaji hayo, Hadi alitoa wito kwa familia kusuluhisha mizozo kupitia mifumo ya sheria iliyopo, badala ya kuchukua sheria mikononi.
Aliwataka watoto kuwatunza wazazi wao, na kuhakikisha wako salama badala ya kugombana nao.
“Ni jukumu la watoto na jamii kuwatunza wakongwe na kuhakikisha wako salama,” alisema Hadi.
Miili ya wawili hao inahifadhiwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi, ikisubiri kufanyiwa upasuaji.