Mmoja wa wawaniaji waliomezea mate tiketi ya chama UDA katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malava, kaunti ya Kakamega amefariki.
Dkt. Enock Andanje aliripotiwa kuzirai na kufariki wakati wa mkutano wa uwezeshaji wajane ulioandaliwa katika eneo bunge hilo leo Ijumaa.
Juhudi za kumfanya arejeshe fahamu katika eneo palipoandaliwa mkutano huo hazikufua dafu.
Ni hali iliyofanya akimbikizwe hospitalini ila alibainika kufariki wakati akiwasili.
Chanzo cha kifo chake bado hakijabainika.
Kiti cha ubunge eneo la Malava kiliachwa wazi kufuatia kifo cha Malulu Injendi mwezi Februari mwaka huu.
Wanasiasa wamekita kambi katika eneo bunge la Malava wakipania kupimana nguvu kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanywa eneo hilo.
Yamkini uchaguzi huo ndio sababu ya Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kukatiza ziara yake nchini Marekani.