Mshukukiwa sugu wa kuwatilia watu dawa za usingizi kwenye vileo na vinywaji katika kaunti ya Mombasa amekamatwa na polisi.
Polisi wamesema mwanamume huyo kwa jina Abdallah Suleiman, almaarufu Asuu, ambaye amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na polisi wa ujasusi, yuko korokoroni.
Hatua ya kukamatwa kwake inafuatia malalamishi mengi yaliyoripotiwa kwenye kituo cha Central cha Mombasa ambapo walevi wengi wamekuwa wakitiliwa dawa za usingizi kwenye pombe na baadaye kuporwa.
Asuu anaaminika kutekeleza uhalifu huo pia kwa wasafiri kuelekea Mombasa, Kisumu na Tanzania na kuibiwa mali zao ikiwemo pesa.
Alikamatwa na polisi katika daraja la kupima uzani wa magari la Mariakani ambapo polisi waliabiri basi lililokuwa likitoka Mombasa kwenda Nairobi.
Polisi walipata dawa hizo kwenye mikoba yake, biskuti, na soda zinazoaminika kutumika kuwapora wateja wake.