Mwanasheria Mkuu wa serikali nchini Tanzania Hamza Johari ameapa kumkamata mwanaharakati Mange Kimambi anayeishi nchini Marekani kwa kuchochea vurugu zilizotokea nchini humo kuanzia Oktoba 29 siku ya uchaguzi.
Johari alisema hayo jana muda mfupi baada ya kuapishwa na Rais wa Samia Suluhu Hassan Novemba 05.2025 kuendelea kuongoza afisi hiyo.
Alisema haiwezekani kwa mtu mmoja kuhamasisha uvunjifu wa amani nchini Tanzania na baadaye anajigamba kwamba ni lazima arejee, jambo ambalo amelitafsiri kuwa ni dharau ya kiwango kikubwa kwa serikali hali isiyokubalika.
“Haiwezekani mtu mmoja amekaa nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dada tu hata ukimuangalia appearance yake, anawaambia watu wakafanye hivyo na wanaenda kufanya kweli, halafu halafu imetokea anaanza kutamba anasema bado nitakuja kivingine, lazima tumkamate” alisema Hamza Johari
Kulingana na mwanasheria huyo, vyombo vya Ulinzi na Usalama vinafuatilia suala hilo kwa namna yake na kama sehemu ya majukumu yao ya msingi na afisi yake pia ina wajibu wa makusudi wa kuhakikisha inalishughulikia.
Hamza alilalamikia kuharibiwa kwa mali za watu binafsi na mali za umma kwenye vurugu zilizotokea nchini Tanzania.
Aliguswa na kuharibiwa kwa gari lake akisema, “Yaani gari la afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali libachomwa moto?, haiwezekani, nimeambiwa kwamba na gari yetu pia imechomwa moto dereva kakimbia”.