Mwanasheria Mkuu asema bado ana mhuri wa serikali

Oduor alisema hakuna kilichobadilika kisheria kuhusu usimamizi wa mhuri wa serikali na hivyo bado uko chini yake.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor amesisitiza kwamba bado mhuri wa serikali uko chini ya ulinzi wake, kinyume na ripoti zilizosambaa awali kwamba ulikuwa umehamishiwa afisi ya mkuu wa utumishi wa umma.

Akizungumza na wanahabari leo Oduor alisema kwamba hakuna lolote limebadilika ikizingatiwa inavyoelekeza sheria kwamba usimamizi wa nembo hiyo muhimu ya serikali uko chini ya afisi ya mwanasheria mkuu.

Mhuri huo ni muhimu kwani ni idhinisho la hadhi ya juu kabisa kwa stakabadhi za serikali.

Utata kuhusu uliko mhuri huo ulitokana na ripoti kwamba ulihamishwa kupitia kwa mswada wa mabadiliko ya sheria za utawala wa kitaifa wa mwaka 2023.

Awali katika mkutano na wanahabari Mei 19, 2025, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alikuwa ametetea hatua hiyo akisema ina msingi wa kisheria unaotambua mkuu wa utumishi wa umma kama msimamizi stahiki wa mhuri huo.

Mei 22,2025, Mwaura alibadili msimamo na kuelezea kwamba mabadiliko yaliyopendekezwa ya kisheria ambayo yangefanikisha uhamisho wa muhuri huo yaliondolewa kwenye mswada husika na hivyo mhuri huo haujahamishwa.

Oduor alisisitiza pia kwamba serikali inatekeleza majukumu yake mbali mbali kwa umoja akipuuzilia mbali dhana ya mgawanyiko serikalini kutokana na suala na mhuri huo.

Share This Article