Kyavaerimukama ambaye wengi wanamfahamu kama Aroma Music ni mwanamuziki wa kike wa Uganda ambaye amekiri kuwahi kugeukia uchawi kama njia ya kuharakisha mafanikio yake katika tasnia ya muziki.
Alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alisema kwamba wakati akianza kazi kama mwanamuziki alilipa mwanamuziki mwenza shilingi laki 5 pesa za Uganda ili amsaidie kwa njia za kishirikina kuafikia umaarufu.
Hata hivyo mwimbaji huyo anasema kwamba baada ya kutoa hela hizo, mambo yake yaliharibika.
“Baada ya kutoa pesa hizo, nilikumbana na shinda zaidi. Ushirikiano wa kikazi niliotarajia haukufanyika na badala ya maendeleo nilikata tamaa” alisema Aroma.
Aroma ambaye sasa anaamini katika ufanisi wa kujituma binafsi alitaja kisa hicho kuwa funzo muhimu maishani mwake kwani sasa amefahamu kwamba ufanisi wa kweli unatokana na talanta, kujitolea na subira na wala sio njia za mkato.
Binti huyo sasa anatumia kisa hicho kuelimisha wanamuziki wengine hasa wanaoanza huku akiwaonya wasiingie kwenye mitego bali waangazie tu kazi zao, watie bidii na waamini katika safari zao.
“Uchawi au njia nyingine za mkato hazitakupeleka mbali” alishauri Aroma.