Mwanamuziki Kalifah Aganaga kuwania ubunge wa Kawempe Kaskazini

Uchaguzi mdogo wa mbunge wa eneo hilo utaandaliwa tarehe 13 mwezi Machi mwaka huu wa 2025, kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa huko.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Sadat Mukiibi maarufu kama Kalifah Aganaga ameteuliwa na chama cha Forum for Democratic Change – FDC kuwania ubunge wa eneo la Kawempe Kaskazini kwenye uchaguzi mdogo.

Chama hicho kimemzindua mwaniaji huyo leo katika makao yake makuu jijini Kampala nchini Uganda.

Chama cha FDC kilikuwa kimeashiria kwamba Aganaga ndiye mwaniaji wake kwa kuchapisha video fupi ya wimbo wake uitwao ‘Ndabirawa’.

Aganaga anajiunga na kinyang’anyiro ambacho kimevutia wengi cha kuchukua mahala pa marehemu mbunge wa eneo hilo Muhammad Ssegirinya.

Mwanamuziki huyo aliwania ubunge wa Rubaga Kusini katika uchaguzi wa mwaka 2021, lakini akashindwa na Aloysius Mukasa.

Tume ya uchaguzi nchini Uganda imetenga tarehe 13 mwezi Machi mwaka huu wa 2025 kuwa tarehe ya uchaguzi huo mdogo.

Mheshimiwa Muhammad Ssegirinya aliaga duniaJanuari 9, 2025 katika hospitli ya Lubaga ambako alikuwa amelazwa kwa muda mrefu.

Ssegirinya ambaye alikuwa mwanachama wa chama cha National Unity Platform – NUP alikuwa mwanasiasa muhimu wa upinzani nchini Uganda aliyejihusisha sana na masuala ya kijamii ya wakazi wa Kampala.

Tume ya uchaguzi imetoa ratiba ya maandalizi ya uchaguzi huo mdogo ambayo inajumuisha usahihishaji wa sajili ya wapiga kura, uteuzi wa wawaniaji na kipindi rasmi cha kampeni.

Chama cha NUP kwa upande mwingine, kitaandaa usaili wa wanachama 10 wanaomezea mate wadhifa huo wa mbunge wa eneo la Kawempe Kaskazini Alhamisi Februari 6, 2024.

Share This Article