Maafisa wa polisi mjini kakamega wanamzuilia mwanamume mmoja kwa tuhma za kumuua mpenziwe katika nyumba ya burudani katika soko la Mbande.
Hali hii iisababsiha simanzi katika kijiji Cha Vuyika eneo bunge la Lugari, kaunti ya Kakamega baada ya familia ya Sivanos Kiliswa kumpoteza mwanawe wa kike, mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Alupe, aliyeuawa katika chumba kimoja cha burudani eneo la soko la Mbande.
Kwa mujibu wa familia, marehemu alikuwa ameondoka nyumbani nyakati za jioni kuelekea sokoni lakini hakurejea.
Baadaye, taarifa ziliibuka kuwa mwili wake ulikutwa ndani ya jumba hilo la burudani na mshukiwa alitoroka mara baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Akizungumza na wanahabari nyumbani kwake, Kiliswa alisema kifo hicho kimemvunja moyo, hasa baada ya kumpoteza mkewe ambaye pia ni mama wa marehemu, wiki mbili zilizopita.
Alieleza kuwa alikuwa na matumaini makubwa kwa mwanawe baada ya kujitahidi kugharimia masomo yake, akiamini angekuwa msaada mkubwa kwa familia katika siku za usoni.
Mmiliki wa jumba hilo la burudani, Farmers Inn, Joash Kubwa, alisema kuwa mfanyakazi aliyekuwa amefika mapema kufanya usafi ndiye aliyegundua mwili wa marehemu.
Chifu wa kata ya Chevanywa, Alex Koricho, alithibitisha tukio huku mwili wa marehemu ukipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Webuye kwa uchunguzi zaidi.