Kwenye duka nambari 31405 katika Soko la Biashara ya Kimataifa la Yiwu, utakutana na mwanamke mmoja mtanashati raia wa China, anayependa kuvalia mavazi ya kitamaduni ya nchi hiyo.
Yeye ni mjasiriamali aliyebobea katika uuzaji wa soksi mbalimbali, zikiwemo zile za michezo.
Nikiwa kwenye pitapita zangu katika soko hilo, nilikutana naye kwenye duka lake linalopatikana katika ghorofa ya kwanza ya eneo la 4, lango nambari 81 kwenye mtaa wa 5.

Wakati huo, Fu Jiangyan, almaarufu Amy, alivalia vazi la kitamaduni la China lenye rangi ya zambarau. Lilishirikiana na tabasamu tulivu lililotamalaki kinywa chake na kumfanya apendeze hata zaidi.
Niliwasili wakati akiwa mbioni kurekodi kitu ambacho sikukifahamu mara moja.
“Yī, Èr, Sān, Sì, Wǔ,” alirudia maneno hayo kwa sekunde kadhaa wakati simu ya mkononi aina ya smartphone ikimkodolea macho.
“Anafanya nini?” nilimuuliza Tony baada ya kukosa subira.
Tony ni Mkenya aliyeishi nchini China kwa kipindi cha miaka 10 na alikuwa mwenye msaada si haba katika kunielewesha utamaduni wa China nilipotembelea mji wa Yiwu.
“Anahesabu moja hadi tano kwa Kichina. Yī ina maana ya moja, Èr ni mbili, Sān ni tatu, Sì ni nne na kisha Wǔ ni tano,” alinielezea Tony.
Mbali na Kichina, Fu pia anaweza akazungumza Kiingereza, hali ambayo hufanya iwe rahisi kwake kuzungumza na wateja ambao ni raia wa kigeni wanaotembelea duka lake.
“Kupitia kwa simu hii, nikitumia teknolojia ya akili mnemba, AI, mimi hurekodi video fupifupi ninazotafsiri katika lugha mbalimbali na kuzisambaza mitandaoni ili kuwafikia wateja wengi duniani,” ananiambia Bi. Fu wakati nikivutiwa na anachokifanya.
“Mimi hutafsiri video hizo katika lugha 36 ambako bidhaa zangu zimepata wateja wengi. Ninakusudia kutafsiri video hizo kwa lugha nyingi hata zaidi kadiri muda unavyosonga.”
Kila video huchukua takriban sekunde 15 kurekodi na chini ya dakika mbili, yeye huwa amemaliza kutayarisha video na kuipachika mitandaoni.
Fu anasema hatua hiyo humvutia wateja wengi na angalau wateja 20 huulizia soksi zake kwa siku.
Nilijaribu kurekodi video hiyo na nilishangazwa kwa sababu ingawa niliirekodi katika lugha ya Kichina baada ya kujifunza lugha hiyo kwa kasi ya umeme, katika kipindi kifupi, ilitafisiriwa katika lugha mbalimbali kikiwemo Kirusi, Kifaransa, na Kihispania.
“Nguvu ya AI imenivutia wateja wengi kutoka kote duniani. Nikiwa papa hapa kwenye duka langu, ninaweza nikawasiliana na wateja kutoka kila sehemu ya dunia kwa lugha wanazofahamu wao wenyewe,” anaongeza Fu ambaye daima huwa mwingi wa furaha.
“Mapato nayo yameongezeka maradufu.”
Si Bi. Fu pekee anayetumia AI kunadi bidhaa zake.
Mnamo mwaka wa 2023, palizinduliwa jukwaa la kunadi bidhaa kwa kutumia AI katika Soko la Biashara ya Kimataifa la Yiwu, linalofahamika kama “China Goods AI Creation Service.”
Kupitia jukwaa hilo, wateja wanaweza wakafahamu uwepo wa bidhaa mbalimbali katika soko hilo na ni eneo lipi zinakopatikana.
Barani Afrika, matumizi ya AI pia yanaanza kushika kasi, ingawa si kwa kiwango cha nchi zilizostawi zaidi kiuchumi na kiviwanda duniani kama vile China.
Pengine katika nchi zinazoendelea kama Kenya, AI inaweza kuwa kifaa muhimu cha kukuza mageuzi makubwa ya kiuchumi na kubuni nafasi za ajira ikiwa itatumiwa ipasavyo na raia wake kuchuma mali ifanyavyo China.
Kwa sasa, katika nchi hizo, AI imetumika sana kueneza habari za upotoshaji na nyakati nyingine kusababisha machafuko, hali ambayo imekuwa chanzo cha miito ya kudhibitiwa kwa mitandao ya kijamii kutolewa.