Mwanaharakati Boniface Mwangi anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo Jumatatu baada ya kukamatwa nyumbani kwake huko Lukenya, kaunti ya Machakos juzi Jumamosi.
Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inaelezea kwamba Mwangi anahusishwa na uwezeshaji wa vitendo vya kigaidi wakati wa maandamano ya Juni 25, 2025.
“Wakati wa kukamatwa kwake, maafisa walichukua simu mbili za rununu, kipakatalishi na vitabu kadhaa vya kuandika,” ilisema DCI kwenye taarifa.
Wapelelezi hao wanasema baada ya kumaliza kutoka nyumbani kwake, walimpeleka Mwangi kwenye afisi yake ya Mageuzi Hub kwenye barabara ya Rose Avenue mtaani Hurlingham.
Baada ya kusaka afisi hiyo, maafisa hao waliondoka na diski tisa za kuhifadhi data, vipakatalishi viwili, sili za kampuni za Brave Media na Courage, muhuri wa kampuni, vitabu sita vya hundi, nakala za hati za ushuru, makopo mawili ya gesi ya kutoza machozi na vingine.
Tangu kukamatwa kwake, Mwangi amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Pangani na anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo Jumatatu.