Mwanaharakati Boniface Mwangi apatikana Ukunda

Alifurushwa Tanzania ambako alikuwa amekwenda kuhudhuria kikao cha kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi ameripotiwa kupatikana huko Ukunda kaunti ya Kwale baada ya kufurushwa Tanzania kwa usafiri wa gari na kuachwa huko.

Kulingana na watu wa familia yake, Boniface alipatikana akionekana mnyonge na alikuwa ameumia na hivyo kupelekwa katika hospitali ya Diani kwa uchunguzi.

Kabla ya hapo Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi ambaye pia ni waziri wa masuala ya nchi za kigeni alikuwa ametangaza kwamba Mwangi ameachiliwa na mamlaka za Tanzania na alikuwa akisafirishwa kwa gari kuelekea Kenya.

Boniface Mwangi ni mmoja wa wanaharakati wa Kenya waliokwenda Tanzania kuhudhuria kikao cha kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini humo CHADEMA, Tundu Lissu.

Wanaharakati wengine akiwemo mwanasiasa na wakili Martha Karua walirejeshwa Kenya wakiwa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere lakini Mwangi alikuwa tayari ameingia Tanzania na aliondolewa kwenye chumba cha hoteli jijini Dar es Salaam.

Jana wanaharakati na watu wa familia yake wakiwemo mke wake waliandamana hadi ubalozi wa Tanzania jijini Nairobi wakitaka Mwangi aachiliwe huru wakisema hajulikani aliko.

Share This Article