Mwanahabari Joyce Gituro leo Jumatatu ameapishwa kuwa Afisa Mkuu wa Mawasialiano ya Umma katika kaunti ya Machakos.
Aliapishwa na maafisa wengine wawili kwenye hafla iliyoongozwa na Gavana Wavinya Ndeti.
“Leo nimeshuhudia kuapishwa kwa Maafisa Wakuu 3 kufuatia kukaguliwa na kuidhinishwa kwao na bunge la Kaunti ya Machakos,” alisema Gavana Ndeti kupitia mtandao wake wa X.
Maafisa wengine walioapishwa ni Francis Munyambu atakayehudumu kama Afisa Mkuu wa Idara ya ukaguzi na Huduma za Dharura na Dkt. Juliana Ndunge aliyeteuliwa kusimamia Idara ya Maji Taka, Usafi wa Mazingira na Usimamizi wa Taka.
“Nachukua fursa hii kuwatakia kila la kheri, uongozi na hekima ya Mungu wanapowatumikia watu wa Kaunti ya Machakos katika kutimiza wito wetu wa Chakula Mezani, Pesa Mfukoni,” aliongeza Ndeti.
Gituro ana tajriba ya takriban miongo miwili katika tasnia ya uanahabari na mawasiliano akiwa amefanya kazi katika vituo kadhaa vya redio humu nchini.