Mwakilishi wadi aliyetoweka arejea

Yussuf Hussein Tolfiyo, mwakilishi wa wadi ya Della iliyoko katika kaunti ya Wajir, alitoweka Septemba 2024.

Marion Bosire
1 Min Read

Yussuf Hussein Tolfiyo, mwakilishi wa wadi ya Della iliyoko katika kaunti ya Wajir, ambaye alitoweka amerejea na kuungana tena na familia yake jijini Nairobi.

Watu wa wamilia yake wamethibitisha kwamba amerejea salama tangu alipotoweka mwezi Septemba mwaka jana.

Habari za kurejea kwake zinajiri miezi kadhaa baada ya mwili uliodhaniwa kuwa wake kupatikana katika Ziwa yahud kaunti ya Wajir lakini vipimo vya msimbojeni yaani DNA vikabaini kwamba sio wake.

Hussein anaripotiwa kuchukuliwa na watu wanaoaminika kuwa watekaji nyara kutoka barabara ya Enterprise jijini Nairobi Septemba 13, 2023.

Katika mahojiano awali, mwanaharakati Bob Njagi aliyetekwa nyara na wengine wawili huko Kitengela Agosti 2024, alisema kwamba mwakilishi wadi huyo alikuwa nao kwenye eneo walilokuwa wamezuiliwa kabla ya kuachiliwa.

Alifafanua kwamba alikuwa kwenye chumba kilichokuwa karibu na kile ambacho walikuwa wamewekwa na watesi wao na yeye alichungulia kwa tundu la ufunguo akamwona.

Share This Article