Mwakilishi wa wadi ya Kariobangi Kaskazini afariki

Joel Munuve anaripotiwa kufariki akiendelea kupokea matibabu katika hospitali moja kwenye barabara ya Kiambu.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwakilishi wa wadi ya Kariobangi Kaskazini katika bunge la kaunti ya Nairobi Joel Munuve amefariki.

Habari za kifo chake zimethibitishwa na spika wa bunge hilo Ken Ng’ondi, ambaye alielezea kwamba Munuve alifariki akiendelea kupokea matibabu katika hospitali moja kwenye barabara ya Kiambu.

Munuve alichaguliwa kwa tiketi huru kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Kulingana na mwakilishi wa wadi ya Kileleshwa Robert Alai kilichosababisha kifo cha Munuve hakijafahamika lakini alilalamikia maumivu akipelekwa hospitalini leo asubuhi.

Alai alielezea kwamba Munuve alichukuliwa kutoka nyumbani na rafiki yake aitwaye Peter na walipokuwa wakielekea jijini Nairobi akalalamika kuhusu maumivu.

“Mipango ya mazishi itatangazwa baadaye. Tunaomba moyo wake ulale salama.” alimalizia Alai.

Katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna ambaye pia ni Seneta wa kaunti ya Nairobi amemwomboleza Munuve akiombea familia yake faraja wakati huu mgumu.

“Maombi yetu ni kwa familia yake kwamba Mungu awatie nguvu. Kwa watu wa Kariobangi Kaskazini, marafiki na viongozi wenzake nasema poleni sana.” alisema Sifuna katika ujumbe wake.

Share This Article