Mwakilishi wa wadi ya Githurai ajiuzulu kisa kutelekezwa

Marion Bosire
2 Min Read
Deonysias Mwangi Waithira na Gavana Johnson Sakaja

Mwakilishi wa wadi ya Githurai iliyo katika gatuzi la Nairobi amejiuzulu akitaja hatua ya eneo analowakilisha kutelekezwa na serikali ya gatuzi hilo.

Katika barua ya kujiuzulu iliyosambazwa mitandaoni, Deonysias Mwangi Waithira anasema alikatishwa tamaa na serikali ya kaunti kwa kukosa kutekeleza huduma muhimu na ahadi za maendeleo kwenye wadi yake.

Kujiuzulu kwa Mwangi aliyechaguliwa kupitia chama cha UDA mwaka 2022, kunaanza kutekelezwa rasmi Novemba Mosi, 2025 na kumechochewa na kile anachokitaja kuwa kutelekezwa kwa eneo lake, kucheleweshwa na uwakilishi mbaya katika utekelezaji wa miradi muhimu ya wadi.

Kwenye barua hiyo ya kujiuzulu ambayo amemwandikia spika wa bunge la kaunti ya Nairobi, mwakilishi wadi huyo alilalamikia hali mbaya ya barabara za wadi yake.

Alitaja barabara za maeneo ya Cifu, Rurii Powerline na Chiro pamoja na mradi uliokwama wa upanuzi wa hospitali ya Githurai Level 3.

Mwakilishi huyo alitaja pia miradi hewa ambayo anasema kwenye stakabadhi za kaunti inaonekana kukamilika lakini haiko na mingine iligharimu mamilioni ya pesa za walipa ushuru.

“Huu umekuwa uamuzi mgumu zaidi kwa maisha yangu,” aliandika Waithira akiongeza, “Lakini siwezi kuendelea kuhudumu chini ya serikali inayotelekeza watu ambao inadai kuwakilisha.”

Alikashifu ukosefu wa uwajibikaji na kuchelewa kwa bunge la kaunti ya Nairobi kutoa fedha za matumizi akisema mambo hayo yamelemaza utoaji huduma kwa watu wake.

Sasa wadi ya Githurai huenda ikaandaa uchaguzi mdogo huku uamuzi wa Waithira ukishangaza wengi na kuibua maswali magumu kuhusu utawala, uwazi wa bajeti na utoaji huduma katika kaunti ya Nairobi.

Share This Article