Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, imetoa ilani ya mvua kubwa inayotarajiwa katika baadhi ya maeneo humu nchini.
Kulingana na Idara, mvua inayonyesha katika baadhi ya maeneo ya Ziwa Viktoria, eneo la Rift Valley, na nyanda za juu Magharibi ya Rift Valley, inatarajiwa kuzidi milimita 20 katika muda wa saa 24 zijazo.
Mvua hiyo itaenea hadi maeneo ya nyanda za juu mashariki mwa bonde la ufa hivi leo, na kuendelea hadi Jumanne, kabla ya kupunguza makali yake Jumatano.
Kaimu mkurugenzi wa huduma za utabiri wa hali ya hewa Edward Muriuki, ametoa wito kwa wakazi katika maeneo hayo kuwa waangalifu, ili kuepuka mafuriko ya ghafla na ukungu.
Wakenya wameshauriwa kuepuka kutembea katika maeneo yaliyo wazi au kujikinga chini ya miti, na kutoketi karibu na madirisha ya vyuma, ili kupunguza uwezekano wa kupigwa na radi.
Muriuki ameonya kwamba mvua hiyo itakayoandamana na upepo mkali huenda ikabomoa paa za nyumba, kung’oa miti na kusababisha uharibifu wa mindo msingi.