Rais William Ruto ametetea muungano wa kati ya vyama vya UDA na ODM, akisisitiza kuwa kamwe hausiani na ugavi wa mamlaka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Ruto amesema ushirikiano kati yake na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga uliosainiwa jana unalenga kuimarisha umoja wa kitaifa ili kukuza utangamano, uchumi, na kubadilisha siasa za nchi.
Aidha, Rais ameongeza kuwa ushirikiano huo wa kisiasa utakabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana, uongozi unaojumuisha Wakenya wote, na kuimarisha uadilifu katika ssekta ya umma kwa kumaliza ufisadi.
Rais amesema haya Jumamosi alipohudhuria mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, Wafula Chebukati, aliyezikwa nyumbani kwake taarafa ya Kiminini kaunti ya Trans-Nzoia.
Marehemu Chebukati aliaga dunia tarehe 20 mwezi uliopita alipokuwa akipokea matibabu ya saratani ya ubingo akiwa na umri wa miaka 63.